Friday, February 3, 2012

MAJUMUISHO


Katika mafunzo ya siku tano yaliyoanza Januari 30 hadi leo Februari 3, sisi kama washiriki na waandamizi katika tasnia ya habari tumepata mafanikio makubwa sana kutokana na mada zilizotolewa na wakufunzi.

Mada kuu katika mafunzo hayo ilikuwa ni jinsi ya kutumia mtandao wa Internet katika kazi za uandishi wa habari na kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi kwa njia ya kisasa zaidi.

Katika mada hiyo tumejifunza na kuelewa jinsi ya kufungua blog zetu wenywe, jinsi ya kutumia blog kwa faida za kitaaluma, kuthibitisha ukweli wa taarifa mbalimbali kwa kutumia mtandao na kufanya uchunguzi kwa kutumia mtandao.

Binafsi nimehamasika kujifunza zaidi jinsi ya kutumia mtandao katika taaluma ya habari na kupata taarifa  toka kila kona ya dunia kwa urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kutokana na mafanikio makubwa niliyopata nitahakikisha nawashirikisha wenzangu kuanzia Ofisini yangu, na wana taaluma kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutumia interenet katika kutafuta taarifa, kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo kutoka vyanzo mbalimbali, kujifunza mambo mapya katika tasnia ya habari na kwenda na wakati kulingana na mabadiliko ya dunia ya sayansi na teknolojia.

Pia nimeongeza uwezo zaidi wa kusoma na kutumia vyanzo vingine bila kuvunja maadili ya uandishi wa habari.
Kutokana na elimu hii naamini utendaji wangu wa kazi utabadilika kwa kuwa nimeongeza ujuzi katika kutafuta taarifa mbalimbali kutoka nje ya nchi kwa njia ya mtandao kwa urahisi zaidi kuliko zamani ikiwemo kuweka baadhi ya taarifa kwenye blog yangu.

Hata hivyo ni wakati muafaka kwa wadau wa habari nchini hususan wamiliki wa vyombo vya haabri pamoja na serikali kuangalia uwezekano wa kutoa elimu hii kwa wana habari nchini badala ya kusubiri misaada kutoka nje kwa kila jambo.

Pia mafunzo kama haya yatolewe kwa waandishi wa habari wengine wa kawaida ambao ndio watendaji wakuu katika vyombo vyetu vya habari kwani bila kufanya hivyo ni sawa na kufundisha Makamishna wa Polisi mbinu za kuzuia uhalifu bila kuwashirikisha askari wa kawaida mbinu hiyo.

No comments:

Post a Comment